.

.

Jumanne, 11 Aprili 2017

1. Ni mambo gani muhimu hufanyika katika vyuo vya Ualimu daraja “A” yanayohusika na kumwandaa mwalimu tarajali wa shule za msingi?
  • Hufundishwa masomo ya saikolojia, falsafa ya Elimu, Misingi ya Elimu, Mitaala na ufundishaji na Njia mbalimbali za kufundisha masomo;
  • Hujifunza kuandaa maazimio ya kazi na maandalio ya somo;
  • Hujifunza taratibu, sharia na miiko ya kazi,
  • Hufanya mazoezi ya kufundisha.
2. Kwa nini saikolojia ni taaluma ya sayansi?
Kwa ujumla saikolojia ni taaluma ya kujifunza tabia na mwenendo wa viumbe, ni taaluma ya kisayansi kwa kuwa huhusika na kujifunza na kupambanua kwa undani mabadiliko ya tabia ya binadamu kutokana na kubadilika kwa vipindi vya ukuaji kwa kiumbe na mazingira anamoishi.
3. Saikolojia ya mtoto ni nini?
Saikolojia ya mtoto ni tawi la elimu linaloshughulikia taaluma ya kujifunza tabia na mwenendo wa mtoto katika hatua mbalimbali za ukuaji wake.
4. Mabadiliko gani yanatokea kwa mtoto kati ya umri wa miaka 2 – 5?
Hiki kinaitwa kipindi cha utoto kwani;
  • Misuli yam tot na neva zake huanza kukomaa na kupevuka,
  • Huanza kufundishwa matumizi ya vitu mbalimbali mfano, choo, kupiga mswaki nk,
  • Huongezeka urefu kwa kasi,
  • Mifupa hukua kwa kasi
5. Lugha ni nini?
Lugha ni chombo cha mawasiliano miongoni mwa binadamu, humsaidia kujenga mahusiano mazuri na wenzake na pia hutumika kufundishia na kujifunza mambo mbalimbali.
6. Taja na fafanua aina kuu tatu za hitilafu ya kuzungumza lugha.
  • Afazia – ni hitilafu katika uwezo wa kutambua na kuelewa maneno yaliyosemwa au kuandikwa na hitilafu katika kubuni maneno ya kuzungumza;
  • Disarthia – ni hitilafu ya kuzungumza inayotokana na mtoto kutoweza kutamka maneno vizuri;
  • Aphonia – hitilafu ambayo mtoto amepoteza kabisa sauti yake.
7. Tofauti ya makuzi na ukuaji wa mtoto
Makuzi kwa mtoto huanza kabla ya kuzaliwa. Mtoto hukaa tumboni mwa mama kwa muda waq miezi tisa au siku kati ya 280 hadi 290 tangu kutungwa mimba. Baada ya kuzaliwa hatua za ukuaji huendelea kwa kupevuka na kukomaa kwa viungo vya mwili.
8. Motisho ni nini?
Katika mazingira ya kujifunza motisho ni kitendo cha kumfanya mwanafunzi ajifunze au awe na ari ya kujifunza. Motisho huhusisha utaratibu wa kutoa vivutio au msukumo Fulani kwa mwanafunzi ili kumfanya ajifunze.
9. Uhawilishaji wa maarifa ni nini?
Ni hali au kitendo cha kutumia maarifa uliyonayo katika kujifunza maarifa mapya.
10. Mtaala ni nini?
Mtaala ni mkusanyiko wa stadi, maarifa na mwelekeo uliopangwa kufundishwa na kujifunzwa na kikundi fulani kwa kipindi kilichopangwa. Pia Mtaala hubainisha kiasi cha maudhui yatakayofundishwa na kujifunzwa na malengo yanayotarajiwa kufikiwa. Maudhui hayo yatakayofundishwa hujitokeza katika muhtasari wa vitendo vya masomo yaliyokubalika.
11. Eleza dhana ya Muhtasari wa somo?
Muhtasari ni mpango wa mambo yaliyopangwa kufundishwa darasani. Pia ni andiko rasmi linalotoa mwongozo wa maarifa, stadi na mwelekeo inayotakiwa kufundishwa kwenye darasa fulani. Mada za muhtasari huonesha mambo ya msingi yanayohusu somo husika. Kwa mfano ujuzi unaotarajiwa kujengwa, malengo mahususi, mada, mbinu za kufundishia na kujifunzia, zana za kufundishia na kujifunzia, upimaji na muda wa masomo kwa wiki.
12. Ni nini tofautisha kati ya Ufaraguzi na Utengenezaji wa zana?
Utengenezaji ni kufanya au kuunda kitu kwa kutumia makunzi halisi. Kutengeneza kunaambatana na michoro, vipimo na makunzi iliyoandaliwa kabla ya uundaji wenyewe kufanyika. Katika utengenezaji muda mrefu unaweza kuhitajika kukamilisha zana unayoitengeneza.
Ufaraguzi ni tendo la ubunifu wa kutengeneza zana papo kwa papo au kutengeneza kwa kutumia makunzi mbadala yanayopatikana katika mazingira husika. Ufaraguzi hauhitaji muda mwingi sana.
13. Vitendeo ni nini?
Ni zana za vitendo vya Elimu ya Awali ambavyo ni vifaa vinavyotumika katika masomo kwa ajili ya kutendea vitendo vya dhana zilizoandaliwa kufundishwa.
14. Orodhesha vitendo sita (6) vya masomo vilivyopo katika muhtasari wa elimu ya awali;
  1. Vitendo vya Hisabati
  2. Vitendo vya Kiswahili
  3. Vitendo vya Sayansi
  4. English learning activities
  5. Vitendo vya Sanaa
  6. Vitendo vya Haiba na Michezo
15. Fafanua uboreshwaji wa Mtaala wa Elimu ya Awali.
Kabla ya uboreshaji wa mtaala wa elimu ya awali wa mwaka 2004, muhtasari wa elimu ya awali ulikuwa na vitendo vya masomo vipatavyo tisa (9) ambayo ni;
  1. vitendo vya Kiswahili,
  2. English learning activities,
  3. vitendo vya michezo,
  4. vitendo vya Hisabati,
  5. vitendo vya Sayansi,
  6. vitendo vya afya,
  7. vitendo vya muziki,
  8. vitendo vya Sanaa na
  9. vitendo vya Haiba.
Baada ya uboreshaji wa mtaala, vitendo vya kujifunza vilipunguzwa hadi kufikia jumla ya vitendo vya masomo sita (6) tu. Mabadiliko hayo yalitokana na kuunganisha vitendo vya Haiba na vitendo vya michezo na kuwa vitendo vya Haiba na Michezovitendo vya Muziki kuunganishwa na vitendo vya Sanaa na kuwa vitendo vya Sanaavitendo vya Afya viliunganishwa na vitendo vya Sayansi na kuwa vitendo vya Sayansi.
16. Fafanua maana ya Elimu linganishi;
Elimu linganishi ni elimu inayoangalia zaidi mfumo wa elimu moja kutoka nchi moja na kulinganisha na mfumo wan chi nyingine katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo katika jamii hususani kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
17. Fafanua neno “Saikolojia” na orodhesha matawi yake.
Saikolojia ni neno kutoka katika tafsiri ya neno la kiingereza lililotoholewa kutoka lugha ya kigiriki linalotokana na muunganiko wa maneno mawili yaani ‘psycho’ likimaanisha akili na ‘logos’ likimaanisha elimu. Hivyo saikolojia ni elimu inayohusu ubongo na mchakato unaotokea ndani yake na jinsi unavyoathiri tabia za kiumbe. Kwa ujumla Saikolojia ni taaluma ya kisayansi inayoshughulikia tabia na mwenendo wa maisha ya binadamu na wanyama.
Saikolojia ina matawi yake ambayo ni;
  1. Saikolojia ya Kijeshi,
  2. Saikolojia ya Biashara,
  3. Saikolojia ya Kliniki/Tiba,
  4. Saikolojia ya Unasihi,
  5. Saikolojia ya Elimu,
  6. Saikolojia ya Elimu Jamii,
  7. Saikolojia ya Makuzi,
  8. Saikolojia ya Watoto na
  9. Saikolojia ya Viwanda.
18. Sosholojia ni nini?
Sosholojia ni sayansi inayohusiana na tabia ya mtu na jamii yake inayomzunguka. Tabia ya mtu inaweza kubainishwa pale mtu anapokuwa katika makundi ya watu ambamo hujifunza mila, desturi na utamaduni.
19. Orodhesha vigezo kumi (10) utakavyotumia katika kuchagua zana ya kufundishia;
Katika uchaguzi wa zana ya kufundishia na kujifunzia ni muhimu kufuata vigezo, Vigezo hivo ni kwamba zana ni lazima inatakiwa kuwa na:
  1. Uimara
  2. Ukubwa unaofaa
  3. Mvuto na kusisimua fikra
  4. Malengo ya somo yahusiane
  5. Kuhusika kwa wanafunzi katika shughuli za kujifunzia
  6. Urahisi wa upatikanaji katika mazingira unamoishi
  7. Umuhimu na ulazima katika kuleta maana
  8. Rahisi kueleweka kwa mtumiaji mwenyewe
  9. Ubunifu katika kutengenezwa
  10. Mwonekano wa kueleweka katika kujifunza
  11. Rahisi kutafsiri mambo mengi yaliyo halisi
20. Taja sifa tano (5) muhimu ambazo za zana za kufundishia na kujifunzia zinatakiwa kuwa nazo;
Zana za kufundishia na kujifunzia zinatakiwa:
  • Zilete maana na makusudio
  • Ziwe sahihi
  • Inatakiwa ziwe rahisi
  • Zisiwe za gharama
  • Zinatakiwa ziwe kubwa zenye mwonekano kwa wanafunzi walio mbali
  • Ziwe za kisasa na zenye kuvutia kama vile rangi
  • Ziweze kubebeka kirahisi
  • Ziweze kuleta motisha kwa wanafunzi
  • Ziendane na umri wa watoto

Maoni 2 :

  1. taja mabadiliko ya mienendo kati ya mwalimu na mwanafunzi

    JibuFuta
  2. 1.kujenga uhusiano mzuri kati ya
    mwalimu na mwanafunzi
    2.kushiriki kwa pamoja katika
    shughuli mbalimbali shuleni
    3.kuwepo na uwazi na ukweli

    JibuFuta

AGGREY TEACHERS' COLLEGE MBEYA

AGGREY TEACHERS' COLLEGE MBEYA

LIKE US ON FACEBOOK

VIEWERS

Aggrey Teachers' College-Mbeya. Inaendeshwa na Blogger.

PAKUA APP YETU HAPA

E-LIBRARY (MAKTABA)

E-LIBRARY (MAKTABA)
SOMA VITABU HAPA.

Popular Posts

*

*

ABOUT

CHUO KIMEJIKITA KATIKA KUTOA ELIMU BORA NA MAFUNZO BORA YANAYOKIDHI MATAKWA YA WATEJA NA KUWA MFANO WAKUIGWA KATIKA UJENZI WA TAIFA. CHUO KIMEFANIKIWA KUWATOA WALIMU WENGI AMBAO WAMETAWANYIKA TANZANIA NZIMA WAKIENDELEZA GURUDUMU LA KULIJENGA TAIFA.
CHUO KIMESAJILIWA NA NACTE KWA NAMBARI REG/TLF/056, USAJILI WAKUDUMU. CHUO KINATOA MAFUNZO YA UALIMU, MAENDELEO YA JAMII NA USTAWI WA JAMII KWA NGAZI YA CHETI NA STASHAHADA.
WASILIANA NASI:-
0754 418 743
0757 412 126
0756 477 090
E-mail: aggreyttc@yahoo.com
Blogsite: www.aggreyteachers'college.blogspot.com